Radio D 1 | Kujifunza Kijerumani | Deutsche Welle

  • Author: Vários
  • Narrator: Vários
  • Publisher: Podcast
  • Duration: 6:18:19
  • More information

Informações:

Synopsis

Paula na Philip ni wahariri wa Radio D wanaochunguza visa vya ajabu. Andamana na wachunguzi hawa shupavu kote Ujerumani na uimarishe Kijerumani chako na uwezo wa kusikiza na kuelewa pia.

Episodes

  • Tukio 26 – Kumuaga Ayhan

    25/08/2009 Duration: 14min

    Hali ya huzuni imetanda katika afisi za Radio D. Ayhan anawaaga wenzake na anarudi nchini Uturuki. Ingawa wafanyikazi wenzake wamemwandalia hafla ya kumuaga, hawana la kuchangamkia. Paula anafika kazini asubuhi na kuwapata watu wote wakijitayarisha kwa sherehe. Hafurahii sherehe hizo kamwe: Ayhan anaondoka Radio D kurudi zake Uturuki kumsaidia baba yake. Katika harakati za kumuaga Ayhan, wafanyi kazi wenzake wameandaa hotuba fupi na zawadi ya kumbukumbu ya rafiki yake Eulalia. Kutokana na hafla hiyo ya kumuaga Ayhan, mwalimu hajishughulishi na sarufi. Hata hivyo anazungumzia maneno machache kuhusu nomino ambatani.

  • Tukio 25 – Kuzikaribisha Meli

    25/08/2009 Duration: 14min

    Waandishi habari hao wanajitahidi kuelewa kauli "getürkt" na wanazuru bandari isiyo ya kawaida ambako kila meli hukaribishwa kwa namna ya kipekee. Katika Bandari ya Willkomm-Höft kila meli hukaribishwa kwa wimbo wa taifa la nchi inakotoka. Kwenye mchezo wao wa redio, Paula na Philipp wanachunguza asili ya mila hii-ambayo yumkini inahusiana na maana ya neno "getürkt." Wakati huo huo, Ayhan anatumia muda wake afisini kusoma vitabu kuhusu bundi. Kwa kuwa Eulalia hajui kusoma, Ayhan anamsomea. Tukio hili linashughulikia zaidi viambishi-awali vya vitenzi na jinsi ambavyo maana ya kitenzi hubadilika pale kiambishi-awali kinapobadilishwa.

  • Tukio 24 – Meza ya Mhariri

    25/08/2009 Duration: 14min

    Bundi Eulalia anawasaidia Paula na Philipp kupata mwelekeo. Wanagundua kuwa wafanyikazi wenzao wa gazeti la Hamburg wanahusika kwenye ulaghai huo. Paula, Philipp na Eulalia wanagundua kuwa wafanyikazi wa gazeti la Hamburg walitunga njama yote ya kuweko papa katika bandari ili wapate kuuza nakala zaidi za gazeti. Baadaye, Philipp na Paula wanazozana kuhusu matumizi ya neno fulani. Philipp anatumai kwamba Paula atatulia pindi akimwalika katika Bandari ya Willkomm-Höft. Lau Philipp angezingatia zaidi maneno aliyotumia, Paula hangeudhika. Kiambishi-awali cha kitenzi kinaweza kuwa kifupi lakini kinaweza kubadilisha maana ya neno. Baadhi ya viambishi vya vitenzi hutenganishwa na kitenzi-jina.

  • Tukio 23 – Pezi la Papa

    25/08/2009 Duration: 15min

    Paula na Philipp wanategua kitendawili cha mahali pa kwenda kumwangalia papa na kwa mara nyingine tena wanagundua ulaghai uliohusika. Hata hivyo mwanzoni sababu za tukio hilo si dhahiri moja kwa moja. Wakiwa katika harakati za kumtafuta mwanamichezo wa kuteleza baharini aliyetoweka, Paula na Philipp wanakutana na mpiga mbizi na hapo wanapata fununu. Mpiga mbizi alikuwa amewahangaisha nusu ya wakazi wa Hamburg kwa kujifunga pezi la papa mgongoni mwake. Wakati huo huo Eulalia amefika Hamburg tayari kusaidia. Pia naye amegundua kitu fulani. Eulalia amepata fununu ambayo huenda ikawasaidia Paula na Philipp- fursa nzuri ya kutumia wakati timilifu. Zingatia zaidi jinsi ya kutumia wakati uliopita hali ya kwendelea.

  • Tukio 22 – Mwanamichezo Aliyetoweka

    25/08/2009 Duration: 14min

    Philipp na Paula wanafuata dalili za papa na kugundua jambo la kushangaza. Wanaingiwa na hamu zaidi wanapopata bao la kuteleza kwenye mawimbi ya bahari bila mwenyewe na pia makala ya gazeti inayowachanganya. Wanapoepukana na zogo la umati wa watu, waandishi habari hao wawili wanachunguza mahali papa alipopatikana. Wanapoona bao lililovunjika la kuteleza kwenye mawimbi ya bahari, wanaingiwa na wasiwasi. Kisha, kwenye gazeti moja la Hamburg wanaona picha ya papa—na wafanyikazi wenzao Laura na Paul ambao wanaonekana kuwa na wasiwasi. Lakini yote hayo yanahusiana vipi? Tukio hili linasisitiza viwakilishi-nafsi "sie" na "er," vinavyotumika pia kuelezea majina ya jinsia ya kike na ya kiume, ambavyo tayari vimezungumziwa.

  • Tukio 21 – Papa katika Hamburg

    25/08/2009 Duration: 13min

    Katika afisi ya Radio D hali ya joto imezidi mno. Paula na Philipp wanafurahi pale wanapopewa kazi ya kwenda pwani ambako papa ameonekana bandarini. Paula, Philipp na Ayhan wanatatizika kwa kiasi kikubwa. Joto limezidi afisini wala hawana kiyoyozi. Paula anatamani kwenda baharini, na Compu anamsaidia kufanya hivyo. Waandishi habari hao wanakwenda Hamburg kwasababu inasemekana papa ameonekana bandarini. Paula na Philipp wanashindwa kupita kutokana na umati wa watu ambao tayari wamefurika kwa nia ya kumwona samaki huyo mkubwa. Mambo pia si rahisi kwa mwalimu ambaye anashughulikia viambishi mwisho vya uhusika wa moja kwa moja wa vidhihirisho vya jinsia ya kiume. Neno la kukanusha "kein" linafuata mtindo sawa wa viambishi vya mwisho.

  • Tukio 20 – Uchunguzi wa Wasikilizaji

    25/08/2009 Duration: 14min

    Paula na Philipp wanawataka wasikilizaji kutoa maoni yao. Mada ya kipindi ni, "Je kusema uongo ni dhambi?" Wasikilizaji wanaweza kutoa maoni yao kuhusu maduara bandia ya mimea na tabia ya wakulima. "Je kusema uongo ni dhambi?" Paula na Philipp wanawauliza wasikilizaji. Swali hilo limetokana na matukio kwenye shamba la mahindi ambayo waandishi habari hao waliyatangaza. Je wakulima walaumiwe kwa vitendo vyao au watalii wanapaswa kujilaumu wenyewe kwa ujinga wao? Wasikilizaji wanaeleza mambo kinagaubaga. Tofauti na waandishi habari ambao wanauliza wasikilizaji maswali ya kujibu "ndiyo" au "la", mwalimu anatoa jukumu lenye uwezekano wa kushughulikiwa kwa jinsi tatu. Nomino za kijerumani zimo katika jinsia tatu: jinsia ya kiume, jinsia ya kike au bila jinsia. Haya yameelezwa katika tukio hilo pamoja na matumizi ya vidhihirisho "der," "die" na "das."

  • Tukio 19 – Kuingilia Jambo kwa Kina

    25/08/2009 Duration: 15min

    Ingawa maduara ya mimea yalitengezwa na Wakulima, Eulalia bado anaamini kuna madude yanayoanguka kutoka angani. Katika kuchunguza ulaghai huo, Philipp na Paula wanakwenda baa ya mahali ambako wanazungumza na wanakijiji. Paula na Philipp wametengua kitendawili cha maduara ya mimea lakini bado wana shaka kuhusu kuweko kwa madude yanayoanguka kutoka angani. Madude hayo ni nini? Eulalia anasisitiza amewahi kuliona moja. Hatimaye waandishi habari hao wanawauliza wateja kwenye baa maoni yao kuhusu maduara bandia ya mimea. Ziara ya baa ni fursa nzuri ya kutanguliza wakati uliopita, hasa kitenzi kisichotabirika "sein" (kuwa). Kitenzi cha utaratibu "können" (kuweza) pia kimeangaziwa katika tukio hili. Zingatia jinsi irabu zinavyobadilika wakati wa kunyambua kitenzi.

  • Tukio 18 – Uchunguzi wa Usiku

    25/08/2009 Duration: 14min

    Paula na Philipp wanataka kujua mbivu na mbichi kuhusu maumbo ya duara ya mimea na wanakwenda usiku kuchunguza. Lakini wanachokumbana nacho hakihusu viumbe kutoka angani. Mwenye shamba lenye maumbo ya duara yasiyoeleweka anawatoza watalii ada ya Yuro 5 kila mmoja ili wapige picha maumbo hayo. Wakati huo huo Philip na Paula wamepiga kambi mwituni kusubiri madude yanayoanguka kutoka angani. Badala yake, wanaume wawili wanajitokeza wakiwa na mtambo. Je wao ndio waliotayarisha hayo maduara ya mimea kuwavutia watalii? Hatimaye, dude kutoka angani linaonekana na hivyo kuzidisha kizungumkuti. Kitenzi "machen" kinaeleweka kwa urahisi. Katika tukio hili mwalimu anakufunza namna tofauti za kutumia neno hili.

  • Tukio 17 – Maduara ya Mimea

    25/08/2009 Duration: 14min

    Paula na Philipp wanakwenda kuchunguza wakati maumbo ya duara yanapogunduliwa kwenye shamba la mahindi. Je kuna dude lililoanguka kutoka angani au kuna mtu anawacheza watu shere? Wakati Ayhna anapowasili katika afisi ya Radio D, nao Paula na Philipp wamo njiani kutoka afisini. Maumbo ya duara yamegunduliwa katika shamba la mahindi na hakuna anayeweza kueleza jinsi yalivyojitokeza. Si waandishi habari hao wawili pekee walio na hamu ya kushuhudia jambo hilo; watalii wengi wanakuja kushuhudia pia. Wakazi wa kijiji hicho wanapata namna ya kujifaidi kutokana na tukio hilo la ajabu. Katika zogo hilo, watu wenye nia tofauti wanajumuika. Watalii wana hamu ya kujionea wenyewe, waandishi habari wanataka kuagua kitendawili hicho na wakulima wanataka kufaidika kifedha. Zingatia vitenzi vya utaratibu katika tukio hili.

  • Tukio 16 – Ikarus

    25/08/2009 Duration: 14min

    Waandishi wote wawili wanashangazwa na kisa cha tanzia cha Ikarus, shujaa wa visaasili vya Kigiriki. Paula na Philipp wanaeleza kisa chake. Paula na Philipp wanapomwona mvulana mdogo amevaa vazi la Icarus wanaingiwa na fikra: Wanaamua kukizungumzia kisa hicho cha Kigiriki kwenye mmoja wapo wa michezo yao ya redio. Kisa chenyewe ni kumhusu kijana ambaye hakufuata nasaha ya baba yake Daedalus na anaanguka anapojaribu kupaa angani. Amezidiwa na tamaa ya kulikaribia jua lakini anapolikaribia nta iliyo kwenye mbawa zake inaanza kuyeyuka. "Usipae juu sana, na usishuke chini sana," Daedalus anamwambia mwanawe Ikarus. Kitenzi cha amri, kilichoshughulikiwa katika tukio hili, kinaweza kutumiwa, kuomba, kuamuru, kuonya au kuagiza. Lau Ikarus alimsikiliza baba yake, pengine hangeanguka.

  • Tukio 15 – Mavazi ya Karnivali

    25/08/2009 Duration: 14min

    Paula na Philipp wanatangaza mara nyingine tena kuhusu Karnivali kutokea barabarani. Wanatambua mavazi tofauti na pia wanajifunza lahaja chache za Kijerumani katika harakati za kazi yao. Afisini Paula analipiza kisasi dhidi ya Ayhan- kwa kutumia taratibu za Karnivali. Kisha kwenye vifijo na nderemo zilizopo barabarani, Philipp na Paula wanatoa taarifa kuhusu mavazi ya asili wanayoyashuhudia. Wanapambana na Papageno kutoka kwenye opera ya Mozart "The Magic Flute" – "Zumari ya Kichawi", na Ikarus, shujaa wa visaasili vya Kigiriki. Philipp na Paula wanakutana na watu wa maeneo mbali mbali ya Ujarumani, wanaozungumza kwa lahaja za kienyeji. Fungua kiungo kilicho chini upate mwongozo wa DW-WORLD.DE wa lahaja.

  • Tukio 14 – Wachawi katika Schwarzwald

    25/08/2009 Duration: 14min

    Hata baada ya kutatizika sana, hatimaye Philipp anafaulu kurudi salama kutoka Schwarzwald na anajitosa kwenye raha ya Karnivali. Paula wala havutiwi na mila hiyo ya Karnivali. Philipp anafurahia sherehe za Karnivali. Paula anaziona sherehe hizo kuwa fujo tupu. Inambidi kumtafuta Philipp na gari lake lililoibwa. Anafanyiwa mizaha na hivyo kutatizika kutimiza lengo lake. Hata Ayhan anamchezea Paula. Matumizi ya kitenzi "sein" (kuwa) ni tofauti kama yalivyo tofauti mavazi yatumiwayo kwenye Karnivali. Katika tukio hili utaangazia vijalizo vya vitenzi tofauti.

  • Tukio 13 – Jumatatu ya Karnivali

    25/08/2009 Duration: 14min

    Si watu wote wanaofurahia Karnivali. Kazi ya Compu inasababisha waandishi habari hao wawili kwenda Schwarzwald ambako Karnivali inachangamkiwa zaidi. Katika baadhi ya maeneo ya Ujerumani watu wanasherehekea Karnivali kwa furaha kubwa. Katika afisi ya Radio D kuna sintofahamu kati ya wahudumu kuhusu sherehe hizo. Paula haoni la kumvutia hata aungane na Philipp kufurahia. Kwake yeye vazi la kichawi alilovaa Philipp ni kichekesho kikubwa. Philipp anafurahia uchunguzi wao unapowaelekeza Schwarzwald ambako watu waliovaa mavazi ya kichawi wanaiba magari katika zaazaa linaloendelea la Karnivali. Waandishi habari hao wanajaribu kuwa na kipindi cha moja kwa moja cha redio lakini wanashindwa. Wachawi wanamteka nyara Philipp baada ya kumburura kutoka kwenye gari. Mpangilio wa maneno katika Kijerumani si jambo la kuchanganya sana. Tukio hili linalenga nafasi ya kiima na kiarifu.

  • Tukio 12 – Barua za Wasikilizaji

    25/08/2009 Duration: 14min

    Endapo kuna jambo usilolijua, ni bora kuuliza. Mwalimu anajibu maswali yaliyoletwa na wasikilizaji wa Radio D kuhusu matukio yaliyopita. Wasikilizaji wanauliza na mwalimu anajibu kila swali kwa kina. Hii ni fursa nzuri kwa wasikilizaji kutafakari taarifa, kupanua ufahamu wao au kuuliza lolote ambalo tangu hapo walinuia kuuliza. Sikiliza maswali haya ya wasikilizaji na majibu ya mwalimu kwa kila swali. Je kiwakilishi gani kinafaa kutumika na kitumike katika hali gani? Wakati gani nitatumia "du" au "Sie"? Wakati gani ninapaswa kutumia jina la kuzaliwa au jina la ukoo? Nini maana ya vishirikishi kama vile "denn", "doch", na "eigentlich"? Nini tofauti kati ya "nicht" na "nichts"?

  • Tukio 11 – Bundi Anayeongea

    24/08/2009 Duration: 14min

    Je jina Eulalia linatoka wapi? Compu, Ayhan na Josefine wanachunguza maana ya jina hilo na kupata maana tofauti. Mfanyi kazi mwenzao mhispania ndiye anayewasaidia. Bundi Eulalia anataka kujua maana ya jina lake. Wahudumu wa afisi ya Radio D wanashughulika kuchunguza na wanagundua asili ya jina hilo ni Ugiriki. Carlos wa idara ya kihispania ana taarifa ya kuvutia kuhusu mada hiyo: Anajua mtakatifu aliye na jina kama hilo. Hata hivyo kundi hilo lina maswali mengi ya kushughulikia. Katika tukio hili utasikia maswali yakiulizwa kwa au bila kutumia maneno ya kuulizia maswali. Kiimbo ni muhimu zaidi.

  • Tukio 10 – Mahojiano na Mfalme Ludwig

    24/08/2009 Duration: 14min

    Philipp anakutana na mwigizaji anayeigiza nafasi ya Mfalme Ludwig katika onyesho la muziki na kumtaka afanye mahojiano naye. Ghafla anatambua sauti yake. Wakati huo huo mgeni asiyetarajiwa atembelea afisi ya Radio D. Katika Kasri la Neuschwanstein, Philipp bila ya msaada wa Paula anafanikiwa kumtambua mtu huyo anayejidai ufalme: ni mwigizaji wa onyesho la muziki la Mfame Ludwig. Philipp anatumia fursa hiyo kumhoji mwanamume huyo. Anaporudi katika afisi ya Radio D mjini Berlin, anashangaa kumpata bundi anayeongea. Tukio hili linaashiria maastajabu anayokumbana nayo Philipp. Utamsikia mara kadha akisema "Das glaube ich nicht" (Hilo siliamini) na "Das weiß ich nicht" (Hilo silijui). Hii ni fursa ya kuzingatia zaidi neno la kukanushia "nicht".

  • Tukio 09 – Muziki wa Ludwig

    24/08/2009 Duration: 15min

    Philipp pia anapata fununu ya kumtambua mgeni. Anaona tangazo gazetini la onyesho la muziki kumhusu Mfalme Ludwig. Akiwa njiani kwenda kwenye ukumbi, anawahoji watalii wanaozuru kutoka maeneo yote ulimwenguni. Huku Paula akiwa afisini mwake Berlin, Philipp naye anahangaika huku na huko mjini Munich. Hana habari yoyote kuhusu jambo aliloligundua Paula, lakini hata hivyo naye anaendelea vyema na uchunguzi wake. Kwenye basi anapoelekea ukumbini anazungumza na watalii kuhusu wanalotarajia kutokana na onyesho la muziki. Fanya mazoezi ya ufahamu wa kusikiliza katika tukio hili. Kwenye basi utasikia lugha nyingi zikizungumzwa. Jitahidi kutambua maneno ya Kijerumani. Utafahamishwa kuhusu neno la kukanushia "nichts" na mahali pake baada ya kitenzi.

  • Tukio 08 – Kumtambua Mgeni

    24/08/2009 Duration: 15min

    Kwenye Kasri la Neuschwanstein, Paula na Philipp wanamhoji mtu anayedai kuwa Mfalme Ludwig. Paula anagundua jambo linalompa fununu ya kumtambua mgeni huyo asiyeeleweka. Waandishi habari hao wawili wanamrai mtu huyo anayedai kuwa Mfalme Ludwig kukubali mahojiano ya moja kwa moja redioni. Hata hivyo asili ya mtu huyo inabaki kuwa kitendawili. Paula anaporejea afisini, anaona tangazo la biashara la runinga linalompa fununu. Sauti ya tangazo hilo si ngeni kwake. Huwezi kuzungumzia vitu unavyohiari bila kusema nini au nani unayempenda. Kitenzi “lieben” huandamana na shambirisho la uhusiano wa moja kwa moja. Katika tukio hili utaelezwa kuhusu uhusika wa moja kwa moja.

  • Tukio 07 – Ludwig, Mfalme wa ajabu

    24/08/2009 Duration: 15min

    Paula na Philipp wanamtambulisha Mfalme Ludwig kwa wasikilizaji kwenye mchezo wao wa redio. Kuteleza thelujini usiku, hafla kubwa na uvumbuzi wa ajabu ni mambo ya mwanzo Ludwig aliyoyafanya katika wakati wake. Waandishi habari hao wawili wanawarejesha wasikilizaji hadi katika karne ya 19. Wanapata habari za Mfalme Ludwig, jinsi alivyokuwa akipenda mandhari asilia, muziki wa Richard Wagner na pia uhusiano wake na binamu yake, Malikia Sissi. Kila mtu anashangazwa na meza ambayo Ludwig aliiunda mwenyewe. Tukio hili linahusu vitu ambavyo Mfalme Ludwig anavihiari, na hivyo inabidi kujifunza kitenzi "lieben" (kupenda). Viambishi-tamati hivyo vinatumika kwa kitenzi "kommen" (kuja), ambacho utakisikia baadaye.

page 1 from 2